5:1-15:21 KUOKOLEWA KUTOKA MISRI
Mkutano wa kwanza wa Musa na Farao (5:1-6:27)
Mkutano wa kwanza wa Musa na Farao ulikuwa wa hasara kwa Waebrania. Farao hakumcha Mungu wao hata kidogo, wala hakuwajali watu wake. Na kwa kweli, Musa alipoomba kibali cha kuwapeleka watu wake jangwani ili wamtolee Bwana sadaka, Farao aliitikia ombi la Musa kwa njia ya kuwalaumu kuwa ni wavivu akawazidishia ugumu wa kazi yao (5:1-14). Jambo hili, licha ya kuzidisha mateso ya Waisraeli, liliwasababisha wamchukie Musa. Mwokozi wao mkubwa hakuwasaidia cho chote, ila aliwazidishia shida tu (15-21)!
Musa alikatishwa tamaa na yale yaliyotokea. Ilionekana kwake kama Mungu alikosa kutimiza ahadi yake. Alimgeukia Mungu, na hapo alitiwa moyo tena (22-6:1).
Mungu alimwambia Musa kwamba maana kubwa ya kuwa BWANA (au YAHWEH), yaani Mwokozi na Mkombozi wa watu wake wa agano, wakati huo ingedhihirishwa wazi kwa watumwa wale walioonewa vibaya kwa jinsi ambavyo haijaonekana kwa watu wakubwa wa nyakati zile. Watu wale, yaani mababu wa Waisraeli, walijua kwamba Mungu alikuwa Mwenye enzi yote, yaani Mwumbaji na Mtawala wa vitu vyote, Yule awezaye kutimiza ahadi zake zote. Lakini walikuwa hawajamwona katika tabia yake ya kuwa Mwokozi wao wa agano, yaani Yule ambaye angewaokoa kutoka utumwa kadiri ya ahadi zake alizompa Ibrahimu (Mwa 15:13-14).
Wakati wa mababu zao, taifa la Israeli halijakuwepo bado. Lilikuwa ahadi kwa wakati wa usoni tu. Kutokana na imani hiyo ya kuwa taifa, maana ya pekee ya YAHWEH (au ya BWANA) ya kuwa Mwokozi na Mkombozi ilisahauliwa pole pole. Lakini wakati huo maana yote ya jina hilo ingedhihirishwa kwa namna ya kutisha sana. Zaidi ya kujifunza jina la Mungu wao tu, Waebrania wangetambua hali na maana iliyodokezwa katika jina la Mungu wao: YAHWEH (BWANA) alikuwa Mungu wa ukombozi (2-8).
Musa alipojaribu kuwaeleza Waisraeli waliokatishwa tamaa mambo hayo, hawakujali hata kumsikiliza. Habari hiyo tena ilimkatisha Musa tamaa, lakini Mungu alimtia moyo na nguvu (9-13).
Orodha ya vizazi iliyoteua vichwa vya nyumba za maana, inaonyesha jinsi Mungu alivyokuwa ameshughulika wakati wa vizazi vya zamani, ili Musa na Haruni wazaliwe wakati huo, ili watekeleze kazi ya kuwaokoa Waisraeli kutoka Misri. Watu hao wawili walikuwa wa kabila la Lawi (14-27).
Unabii wa hukumu iliyokaribia (6:28-7:13)
Kabla Musa hajamkaribia Farao tena, ili kumpa nafasi ya mwisho ya kuwapa Waisraeli uhuru, Mungu alimkumbusha Musa kwamba, siyo Farao peke yake tu, bali taifa lote la Misri lilikuwa katika hatari ya hukumu. Watu wote pamoja na mfalme wao walikuwa wakaidi wakimpinga BWANA, pia walikubali kuwafuata maadui wa BWANA, yaani miungu ya Misri (6:28-7:7; taz.9:27; 12:12).
Miungu ile ilikuwa ya viumbe vya ulimwengu, na hivyo ilihusika na Mto Nile uliokuwa tegemeo lote la Misri kwa maji yake, na kwa mbolea iliyokuwa katika matope ya maji yake yaliyofurika katika mashamba kila mwaka. Kufuatana na imani ya Wamisri, miungu ile ndiyo iliyoleta mafanikio na ustawi. Itaonekana kwamba mapigo yaliyoletwa na Mungu yalikuwa hukumu juu ya miungu ile. Mapigo yalikaziwa zaidi katika bonde la Nile, nayo yalileta uharibifu na magonjwa yaliyoenea sana (10:2).
Mungu alimpa Farao nafasi ya mwisho ya kuwapa Waisraeli uhuru kabla ya kuanza na mapigo. Lakini wachawi na wataalamu wake walipoweza kutumia akili zao na kuiga ishara za Musa na Harani, Farao aliwadharau viongozi wa Kiebrania na kuwafukuza(8-13).
Mapigo tisa (7:14-10:29)
Wakati, ukali na maeneo ya mapigo yale vinaonyesha wazi kwamba vilitoka kwa Mungu. Pia inaonekana kwamba Mungu alitumia hali ya asili ya bonde la Nile ili kuleta mapigo hayo. Pigo la kwanza lilichafua maji ya Nile, mitaro yake na mabwawa yote yaliyounganika nayo. Matokeo yake samaki wote wakafa. Mizoga ya samaki ilipopelekwa kando ya mito na mifereji, vyura wote walitoka majini, na hivyo pigo la pili lilitokea. Wachawi wa Misri waliweza kumwiga Musa katika mapigo mawili ya kwanza, ingawa baada ya kuona maji yote yalivyokuwa mekundu kutokana na vyura, uwezo wa wachawi haukuwashangaza watu zaidi. Kama wangaliweza kuondoa mapigo yale, wangaliwasaidia watu na Farao, lakini hawakuweza. Kwa njia hiyo wangaliweza kuonyesha nguvu yao, ila walishindwa (kama vile fimbo ya Haruni iliyobadilika kuwa Nyoka na kuwameza nyoka wengine). Mungu peke yake alitawala mambo, na Musa alithibitisha hayo kwa Farao alipowaondoa vyura wakati ule ule alioutangaza kabla (7:14-8:15).
Mungu alipotia mkazo zaidi katika kuonyesha mamlaka yake kwa mfululizo wa mapigo, wachawi wa Misri walikubali kwamba Musa na Haruni hawakuweza kulinganishwa na wachawi na waaguzi walioweza kutabiri mambo ya usoni tu, na kisha kufanya ujanja fulani ili mambo yale yatokee, kusudi waweze kusema kwamba wao walioyaleta. Wachawi walilazimishwa kukubali kwamba walishindwa. Habari ya kuwa Waisraeli hawakuguswa kabisa na mapigo hayo, ilikuwa thibitisho lingine kwamba Mungu mwenyewe alileta mapigo hayo naye aliyatawala. Hali ya pekee ya kuzaana kwa vidudu iliyotokana na mapigo mawili ya kwanza, inaweza kuwa sababu ambazo Mungu alizitumia kwa kuleta mapigo yaliyofuata, yaani ya chaw a na mainzi wabaya(8:16-32).
Kutokana na mafungu mengi ya mizoga ya vyura waliooza juani, na mainzi walioeneza uchafu wao, pigo lingine halikuchelewa lililoleta maafa makubwa katika wanyama wa nchini kote (isipokuwa wanyama wa Waebrania) ambalo lilifuatwa na pigo lingine la ugonjwa mkali wa ngozi ya wanadamu (9:1-12).
Kabla ya kutangaza pigo la saba, Mungu alimkumbusha Farao huruma yake kwake katika mapigo yaliyopita. Mungu angaliweza kumwangamiza pamoja na watu wake katika pigo moja kubwa sana, lakini badala yake alituma mapigo madogo, na kila mara alimpa Farao nafasi ya kutubu. Kwa kadiri ambavyo Farao angechelewa kutubu, anguko lake lingekuwa kubwa zaidi, na utukufu wa Mungu ungezidi, na mwisho Farao angepinduliwa kabisa. Mungu alitoa maonyo ya kutosha kabla ya kutokea misiba ya mvua ya mawe na ngurumo yenye radi, ili watu waliotaka kujiokoa katika pigo hilo waweze kufanya hivyo. Watumishi wengi wa Farao waliomwogopa Mungu wa Israeli, walisikiliza onyo la Musa, hatimaye waliukwepa msiba huo (9:13-35).
Wakati huo kulikuwa na mfarakano kati ya watumishi wa Farao. Baadhi yao waliendelea kuwa na ukaidi na kumsikiliza Farao, lakini wengine walijaribu kumshauri awape Waisraeli uhuru. Hivyo Farao aliwapa Waisraeli masharti yasiyokubalika kwao, na maafa mengine yakatokea. Shayiri na kitani tu vilikuwa vimeangamizwa katika pigo la saba. Ngano ambayo msimu wake ulikuwa bado, iliangamizwa na nzige wakati wa pigo la nane (10:1-20).
Inawezekana kwamba pigo la tisa lilikuwa dhoruba kali ya mavumbi yaliyokuwa mengi mno, kiasi kwamba jua halikuonekana, nchi yote ikawa na giza nene. Mavumbi yalizidi na giza liliweza kushikwa kwa uzito wake. Mpaka wakati huo Farao alikuwa hajataka kuwarahusu Waisraeli bila masharti fulani. Musa aliona wazi kwamba wakati wa kujadiliana naye ulifikia mwisho wake (10:21-29).
Kutangazwa kwa pigo la mwisho (11:1-10)
Ingawa onyo la kutosha lilitolewa kwa pigo la mwisho, wakati wake halikutajwa. Lakini Waisraeli waliagizwa wajiandae kwa safari yao ya kuondoka Misri, kwa sababu pigo hilo halikuwa hukumu kuu ya mwisho kwa Wamisri tu, bali pia lilikuwa tendo kuu la ukombozi kwa watu wa Mungu (11:1-3; kwa habari ya mistari ya 2-3 taz. maelezo ya 3:21-22). Pigo hilo lingewaua wazaliwa wa kwanza wote wa wanadamu na wa wanyama katika nchi yote ya Misri. Lingetimiza onyo alilopewa Farao hapo awali (4-10; 4:22-23).
Pasaka (12:1-36)
Mpaka wakati huo Waisraeli hawakupatwa na hukumu za Mungu za mapigo, wala hawakudaiwa kufanya jambo lo lote la kujikinga, lakini wakati huo usalama wao ulitegemea utii wao kwa maagizo ya Mungu. Ukombozi unawekewa sharti la imani na utii.
Kila nyumba ingeokolewa katika hukumu kwa njia ya kuchinja sadaka ya mnyama, na damu ya mnyama huyo ipakwe katika mlango wa nyumba ambamo familia hiyo iliishi. Damu hiyo iliyopakwa mlangoni iliwaonyesha watu wa nje kwamba sadaka ya naibu ilitolewa, yaani maisha ya mnyama yalitolewa maisha ya mzaliwa wa kwanza. Hivyo mwuaji wa BWANA 'angeipita' nyumba hiyo, na ndani yake asingeuawa mtu (maana ya neno Pasaka ni 'kupita').
Karamu ya Pasaka iliyofuata ilitakiwa iandaliwe kwa jinsi isivyopoteza muda. Kwa sababu hiyo mnyama hakutakiwa kukatwa vipande na kuchemshwa, bali aokwe juu ya moto wazi na mikate yake itengenezwe bila chachu (au hamira), ili kuokoa wakati wa kungojea mpaka mkate uumuke. Ilitakiwa kuwa karamu rahisi, iliwe kwa haraka, na watu wawe wamevaa kabisa kuwa tayari kuondoka asubuhi. Ilikuwa marufuku kusaza nyama yo yote mpaka asubuhi, labda kwa kuzuia kuharibika kwake, pia labda kwa kuzuia sehemu yake isitunzwe kwa namna yo yote ya dawa. Hali ya kuwa bila mapambo yo yote katika karamu na heshima yake, bila shaka iliwazuia Waisraeli wasijisifu wala kujitukuza wenyewe (12:1-14).
Katika juma lililofuata watu wasingekuwa na nafasi ya kutengeneza mikate yenye chachu na kungoja mpaka iumuke. Kwa hiyo walitakiwa wachukue donge na vyombo vya kuokea pamoja nao, ili waweze kuoka mikate yao njiani. Wakati wote wa usoni katika historia ya Israeli, watu wasisahau kamwe habari ya kuondoka kwao Misri kwa haraka. Matendo ya mfano wa Pasaka pamoja na karamu ya mikate isiyotiwa chachu, yaliagizwa yaadhimishwe katika sikukuu ya kila mwaka, ili kuwakumbusha Waisraeli habari za kuokolewa kwao kutoka utumwa (15-36; taz.Mk 14:1).
Waisraeli waondoka Misri (12:37-51) Ilikuwa kama miaka 430 hivi baada ya Yakobo kuhamia Misri, wazao wake walioongezeka kuwa taifa kubwa walipoondoka Misri tena (Mwa 15:13; 46:6-7). Kundi kubwa la watu wasiokuwa Waisraeli, pamoja na Wamisri na wengine waliooana na Waisraeli au kuchangamana nao tu, pia walisafiri pamoja nao kutoka Misri (37-42). Waisraeli hawakutakiwa kuwarudisha watu hao, wala wasilegeze maagizo na kanuni zao walizopewa na Mungu kuhusu sherehe mbalimbali za dini na sikukuu zake kwa ajili ya nafuu ya wageni hao. Kinyume chake, wageni hao walipaswa kutimiza maagizo yote ya agano na kushirikiana nao kama waabudu wa BWANA, aliye Mungu wa kweli (43-51).
Kuwekwa wakfu kwa wazaliwa wa kwanza (13:1-16)
Mungu aliwaokoa wazaliwa wote wa kwanza wa Israeli na wanyama wao katika hukumu ya Pasaka. Kwa sababu hiyo wazaliwa hao wa kwanza walikuwa mali na haki ya Mungu. Watu waliagizwa watambue jambo hili na kuwaweka wakfu (maana yake ni kuwaweka kando kwa ajili ya Mungu) wazaliwa wao wa kwanza katika sherehe ya ibada ya kumshukuru Mungu (13:1-2; taz.mst. 15). Tendo hili liliweka mfano wa kuwekwa wakfu kwa taifa lote la Mungu, kwa sababu Israeli kwa jumla lilikuwa mzaliwa wa kwanza wa Mungu (taz.4:22). Tena watu walikumbushwa kutekeleza sherehe ya sikukuu ya Pasaka na Mikate isiyotiwa chachu, kwa sababu tukio ambalo siku hiyo ilikuwa kumbukumbu lake, lilikuwa sababu ya kuwekwa wakfu kwa wazaliwa wa kwanza (3-10).
Wanyama waliohesabiwa kuwa safi au halali, kama vile kondoo, mbuzi na ng'ombe, waliwekwa wakfu kwa Mungu kwa njia ya kuwa dhabihu. Wanyama waliokuwa haramu, kama vile punda n.k., wasiofaa kuwa dhabihu, walipaswa kukombolewa, maana yake wakombolewe kutoka kwa Mungu kwa malipo ya wanyama wengine waliokuwa halali kuwa dhabihu, ili wawe naibu yao. Kama hawakukombolewa walipaswa kuuawa hivi hivi. Lakini kumtoa mwanadamu kuwa dhabihu ilikuwa marufuku. Kwa habari ya wazaliwa wa kwanza wa wanadamu, wao walitolewa kwa Mungu katika sherehe maalumu, kisha wakakombolewa tena kutoka kwa Mungu kwa njia ya kulipa kiwango fulanichapesa(ll-16;taz.Hes 18:15-16).
Maelezo: Lugha ya kimfano ya 13:9,16 iliyonena habari za umuhimu wa dini ya kweli katika maisha ya mtu rohoni mwake na ya matendo yake ya nje, ilitafsiriwa moja kwa moja na Wayahudi wa baadaye, na kwa matokeo yake walitengeneza vitu vilivyofanana na hirizi. Vitu vile vilikuwa vijikasha vyenye vipande vya nguo ambavyo juu yake mistari hii na mingine iliandikwa. Kwa kawaida Wayahudi walivaa vijikasha vile katika mikono yao au katika vipaji vyao (Mt 23:5).
Ushindi wa mwisho juu ya Misri (13:17-14:31)
Waisraeli walipoondoka Misri, hawakushika njia fupi ya karibu na pwani ya Bahari ya Kati, kwa sababu njia ile ililindwa vikali na majeshi ya Wamisri, na bila shaka wangalishambuliwa nayo. Badala yake walikwenda mashariki kuelekea Bahari ya Shamu. (Haikuwa Bahari ya Shamu tunayoita Bahari ya Shamu siku hizi, bali tafsiri yake halisi ni Bahari ya Matete iliyokuwa nyongeza ya kaskazini ya ghuba ya Suez.)
Waisraeli wakiongozwa na ishara za uwepo wa Mungu, walielekea Kanaani. Walichukua pia maiti ya Yusufu iliyohifadhiwa kwa dawa isije ikaoza. Yusufu alikuwa ameagiza hivyo hapo awali, na kwa njia hiyo alionyesha imani yake kwamba siku moja watu wake wangerudi katika nchi ya ahadi (17-22; Mwa 50:25; Ebr 11:22).
Kinyume cha imani ya Yusufu, Waisraeli hawakuonyesha imani walipotambua kwamba waliongozwa mahali pasipokuwa na njia ya kutoka; yaani maji yalikuwa mbele yao, na askari wa Misri walikuwa nyuma yao waliotaka kuwaua, na kila upande hali ya nchi ilikuwa mbaya sana, hata wasiweze kutoroka (14:1-12). Lakini Musa aliona mambo yote kuwa chini ya utawala wa Mungu. Mungu alikuwa amemvuta Farao atoke nje. Wakati huo angetukuzwa katika tendo moja kubwa ambalo lingeleta hukumu ya mwisho juu ya Misri, na wokovu kamili kwa watu wake (13-18).
Jua lilipokuchwa siku ile Wamisri waliwakaribia sana Waisraeli, nusura kuwapata, lakini wingu lile la moto lililokuwa mfano wa uwepo wa Mungu, liliingia katikati ya makundi yale mawili, likawazuia Wamisri wasiendelee mbele zaidi (19-20). Upepo mkali uliotokea uliendelea usiku kucha ukawasaidia Waisraeli kwa kukausha bahari kiasi cha kutosha, ili njia iwepo kwa Waisraeli kuvukia upande wa pili. Mara kabla ya kupambazuka, Waisraeli wote walipokuwa wamevuka, Wamisri walijaribu kuvuka vile vile, lakini wakati huo upepo ulitulia, na maji ya bahari yalirudi katika hali yake ya kawaida. Hali hiyo kwanza iliwaletea Wamisri wasiwasi, kisha hofu ya ghafla, na mwisho iliangamiza kabisa jeshi la magari la Wamisri (21-29). Kuingilia kati kwa Mungu kuliwashinda maadui, na wakati huo huo kuliwanyenyekeza Waisraeli, ili wapate tabia mpya kabisa ya imani na uchaji wa Mungu (30-31).
Wimbo wa ushindi wa Musa (15:1-21)
Wimbo ulioimbwa na Musa na watu wake ulikuwa zaidi kuliko wimbo wa furaha tu juu ya adui aliyeshindwa. Zaidi ya yote ulikuwa wimbo wa kumsifu Mungu ambaye tabia na hali yake vilidhihirishwa, na watu wake walipata kuvitambua zaidi katika matukio ya kuokolewa kwao kutoka Misri. Yeye alikuwa Mungu mwenye nguvu na mamlaka aliyewaokoa watu wake na kuwapindua maadui zao. Kweli, alikuwa Mungu mwenye utukufu wa kutisha na mwenye utakatifu aliyeweza kuongoza nguvu za asili ya ulimwengu, hata waasi na wenye kiburi waangamizwe kabisa (15:1-10). BWANA alitekeleza hukumu yake juu ya miungu ya Misri. Zaidi ya hayo, alikuwa Mkombozi wa agano la Israeli, naye alikuwa mwaminifu kwa ahadi zake (11-13; taz.6:6;12:12).
Zaidi ya hayo, ushindi uliwapa Waisraeli matumaini kwa wakati wao wa usoni. Kama walivyokuwa wamewaona Wamisri wakiangamia pamoja na mamlaka na majeshi yao yote, vivyo hivyo walitazama mbele na kuona mataifa yasiyokuwa na nguvu namna hiyo wangeyakuta njiani kwenda Kanaani, nayo yangeshindwa vivyo hivyo. Baada ya kuwaokoa katika utumwa, kwa hakika Mungu angewapeleka katika nchi yao ya ahadi (14-18). Kisha Miriamu aliwaongoza wanawake katika sherehe ya ushindi katika muziki, michezo na kuimba nyimbo (19-21).