1:1-4:31 MAANDALIZI YA MUSA

Kunyanyaswa kwa Israeli (1:1-22) Familia ya Yakobo iliyohamia Misri hapo awali ilikuwa jumuia ndogo tu. Siku za kwanza za watu wale huko Misri zilikuwa za furaha na mafanikio (Mwa 46:1-7; 47:11-12). Mungu alikuwa ameahidi kwamba wangekuwa taifa, na katika karne zilizofuata waliongezeka sana katika idadi na katika ushawishi wao, hata wakajaza karibu sehemu yote ya kaskazini-masharikiya Misri (1:1-7; Mwa 13:16; 17:2;47:27). Wakati huo watawala wa Misri hawakuwapenda Waisraeli (au Waebrania walivyoitwa na Wamisri). Farao aliogopa kama maadui wangeshambulia maeneo yao, Wairaeli wangejiunga nao, na hivyo aliamua kuwatawala Waebrania yeye mwenyewe kwa dhati zaidi. Aliwalazimisha kufanya kazi ya utumwa, ili wajenge na kuimarisha miji ambayo Wamisri wangeweza kuitumia kwa kuwekea akiba ya silaha kwa majeshi yao (8-14). Farao pia alijaribu kutawala uzazi wa Waebrania wasije wakaongezeka zaidi, kwa njia ya kuingiza siasa ya kuwaua watoto wachanga wakati wa kuzaliwa kwao. Lakini makusudi ya hila zake hayakuwezekana, kwa sababu ya ujasiri wa baadhi ya wakunga waliowasaidia Waebrania katika kuzalisha. Wao walimcha Mungu kuliko Farao. Katika mambo hayo yote Mungu alifanya kazi yake, akiwahifadhi watu wake kwa kadiri ya ahadi yake ya agano (15-22).


Maandalizi ya Musa (2:1-25) Musa alikuwa mtu aliyechaguliwa na Mungu ili awaokoe watu wake na kuwaongoza kutoka Misri. Alizaliwa na wazazi wa Kiebrania waliomcha Mungu. Hao bila mashaka yo yote walimwambia kwamba kuna Mungu wa kweli aliye hai ambaye watu wanapaswa kumwabudu na kumtegemea peke yake, naye ndiye aliyechagua Israeli kuwa taifa lake. Lakini wakati huo huo Musa alilelewa katika makao ya mfalme wa Misri ambako alifundishwa elimu na ustaarabu bora uliopatikana katika ulimwengu wa wakati ule (2:1-10; taz.Mdo 7:22; Ebr 11:23).


Musa alipofikia umri wa miaka 40, alipata uhakika kwamba Mungu alimchagua ili awaokoe Waisraeli katika utumwa wao wa Misri; lakini tendo lake la haraka la kumwua Mmisri aliyempiga Mwebrania, lilionyesha kwamba alikuwa hajawa tayari kwa kazi aliyokusudiwa na Mungu. Wala watu wake hawakuwa tayari kumtambua yeye awe mwokozi wao kwa wakati huo. Kwa ajili ya kuokoa maisha yake, Musa alipaswa kutoroka Misri, na alipofanya hivyo alikataa moja kwa moja na kwa makusudi kabisa hali yake na cheo chake cha Misri (11-15; Mdo 7:23-29; Ebr 11:24-25).


Nchi ya Midiani aliyokimbilia Musa, ilikuwa nchi ya ukame, na inafikiriwa kwamba ilikuwa upande wa mashariki ya Misri katika mkono wa nchi ya Sinai. (Wamidiani walikuwa wazao wa Ibrahimu kwa njia ya suria wake Ketura, na hivyo walikuwa jamaa wa mbali wa Waebrania, Mwa 25:2-4). Kwa miaka mingi Musa aliishi katika nyumba ya mkuu mmoja wa Midiani, jina lake Reueli (ambaye pia aliitwa Yethro), na binti yake alikuwa ameolewa na Musa. Hapo bila shaka Musa alijifunza mambo mengi kuhusu maisha ya jangwani, ya jumuia na ya utawala wa kikabila ambayo yaliweza kumfaa baadaye alipowaongoza Waisraeli katika safari yao ya kwenda Kanaani (16-22).


Musa aliishi Midiani kwa muda wa miaka 40 (Mdo 7:30). Wakati ule wote Waebrania huko Misri waliteswa na kunyanyaswa vibaya sana, lakini wakati ule wote Mungu alikuwa akimwandaa Musa ili awaokoe. Mungu alimfundisha Musa mambo yaliyotakiwa ili afaulu kuwaokoa watu wake kutoka utumwa wa Misri na kuwapeleka katika usalama wa nchi yao mpya waliyoahidiwa. Mambo aliyofundishwa ni hayo: Kujitawala, kuwa hodari, kutii na kumtegemea Mungu (23-25).


Mungu amwita Musa (3:1-12)

Musa alipowachunga kondoo karibu na Mlima Sinai (ulioitwa pia Mlima Horebu, kufuatana na eneo la malisho yaliyokuwepo huko), Mungu ambaye kwa muda wa miaka 80 alikuwa ameongoza maisha yake kwa siri, alijijulisha kwake mara ya kwanza. Mafunuo ya Mungu katika kichaka kilichowaka moto yalionyesha kwamba, ingawa Mungu huyo alikuwa mtakatifu, wala haikuwezekana kumkaribia, aliweza kukaa katika vitu vya kidunia bila kuviangamiza (3:1-6).


Wakati huo Mungu alikuwa tayari kuwaokoa watu wake kutoka utumwa wa Misri, naye alitaka kumtumia Musa kuwa mwokozi wao. Baada ya kuchukua hatua ya kwanza ya imani ya kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri na kuwaleta ili waabudu katika Mlima Sinai, Musa angeimarishwa katika imani yake. Wakati huo angejua hakika kwamba Waisraeli wangewashinda maadui zao wote na kuteka nchi yao waliyoahidiwa (7-12).


Mungu wa Israeli (3:13-22) Kama Musa alitakiwa kuwa mjumbe wa Mungu kwa Waisraeli ambaye angewaongoza kutoka Misri, angepaswa kuwahakikishia kwamba alijua makusudi ya Mungu kwa ajili yao. Lakini alikuwa na wasiwasi kama wangemwelewa, kwa sababu hawakujua tabia ya Mungu yule ambaye walijua tu kwamba ni Mungu wa wazazi wao, lakini siyo zaidi. Musa alipomwomba Mungu amsaidie kuwaeleza Waisraeli makusudi yake, hakutaka kujua jina lake tu, bali pia tabia yake mwenye jina hilo (13).


Mara nyingine, Mungu alipotaka kujidhihirisha upya, alijidhihirisha kwa jina la cheo kipya kilichojumlisha ufunuo wake kwa neno moja au mawili. Jina lake ambalo Mungu alimdhihirishia Musa wakati huo lilikuwa 'MIMI NDIMI’.


Jina hilo la 'MIMI NDIMI’ pamoja na maneno machache ya kulieleza lilitakiwa kuwa la siri, kwa sababu Mungu hakutaka kuridhisha udadisi, bali alitaka kujijulisha kwa wale waliotaka kumjua hasa. Jina lake lilidokeza tabia ambayo ingefunuliwa katika matukio makuu ya ushindi. Mungu wa milele, asiyebadilika, aliopo pote na wakati wote, ashughulikaye pote na wakati wote, angethibitisha kwamba watu wangeweza kumtegemea siku zote, naye angeweza kabisa kutoa kila kitu kinachohitajiwa na watu wake. Yeye angekuwa ye yote Yule, ili athibitishe kwamba angefaa kwa kila hali ambayo ingewakuta Waisraeli (14-17).


Ingawa baada ya muda Musa angekubaliwa na Waisraeli, angekabiliwa na ukaidi wa mfalme wa Misri. Farao angekataa maombi ya Waisraeli ya kwenda mbali kidogo, ili wamwabudu Mungu wao bila ya kuwa chukizo kwa Wamisri (8:26-27), na hivyo angeonyesha hali na tabia yake hasa. Nguvu na mamlaka ya Mungu ya kushinda ukaidi na kiburi chake, vingeonyeshwa kwa namna ya ajabu sana. Hata Wamisri wangewapa Waebrania utajiri wao kwa furaha (yaani deni waliyowiwa na Waebrania baada ya miaka mingi ya kazi ya utumwa), ili waondokane nao (18-22; 12:33-36).


Jina la Mungu

Mababu wa Waisraeli walimjua Mungu kama 'BWANA', YAHWEH (au Yehova)(Mwa 2:4; 12:1; 26:2; 28:21; 49:18), lakini jina hilo halikuwa na maana sana kwa Waisraeli wa wakati wa Musa. Ufunuo wa Mungu kwa Musa kwa jina la 'MIMI NDIMI’ katika Kutoka 3:14 ulikuwa maelezo ya maana ya jina YAHWEH kwa watu wa Mungu.


Katika lugha ya Kiebrania neno lililotafsiriwa 'MIMI NDIMI' lilihusiana na jina la YAHWEH. Hapo mwanzo katika Kiebrania herufi za konsonanti tu ziliandikwa na herufi za vokali zilitamkiwa wakati wa kusoma tu. Inaaminiwa kwamba 'YAHWEH' ni sawa kwa neno la YHWH (yaani jina la Mungu wa Waisraeli), ingawa uhakika kabisa haupatikani, kwa sababu Kiebrania cha kale kabisa hakipatikani siku hizi. Wakati vokali zilipoingizwa katika maandishi ya Kiebrania, Wayahudi walikwisha acha kutamka jina la YHWH. Wao walidai kwamba hivyo walionyesha heshima kwa jina takatifu la Mungu, lakini wengi wao waliogopa tu kulitumia. Kwa hali yo yote Wayahudi walijenga desturi ya kutumia jina la Adonai (maana yake 'Bwana') badala ya YHWH waliposoma Maandiko yao.


Vokali zilipoingizwa katika Biblia ya Kiebrania mara ya kwanza (kama miaka 300 k.K.), vokali za adonai ziliongezwa katika konsonanti za YHWH.


Hivyo neno la Yehova lilipatikana, ingawa Wayahudi waliendelea kutumia adonai katika usemi wao. Watafsiri wa lugha za kisasa kwa kawaida waliepukana na shida ya utamshi wakatumia neno 'BWANA' (katika herufi kubwa) badala ya YHWH.


Mungu ampa Musa nguvu (4:1-17)

Musa aliendelea kulalamika kwa Mungu akisema kuwa Waebrania wasingeamini kwamba alitumwa naye, na hivyo Mungu alitnwezesha kuonyesha ishara tatu za ajabu. Waebrania waliozoea maajabu ya wachawi wa Misri, wangezistaajabia, lakini wangeona kwamba miujiza ya Musa ingekuwa zaidi kuliko uchawi wa Misri (4:1-9).


Lakini hata Musa mwenyewe mara nyingine alionyesha dalili ya kutoamini, kama vile alivyokuwa ametia wasiwasi kwa Waebrania wenzake. Kama neno lake kwamba hakuweza kunena lilikuwa kweli au siyo, tabia yake ilionyesha ukosefu wa imani. Alikuwa akijitafutia udhuru tu, na jambo hili halikumpendeza Mungu. Matokeo ya malalamiko yake yalikuwa kwamba, Mungu alimchagua kaka yake, Haruni, ili awe msemaji wake (10-17).


Musa arudi Misri (4:18-31)

Baada ya kukutana na Mungu, Musa alimrudia mkwewe, Yethro, akawatwaa mke na wanawe wawili akaenda Misri. Mungu alimwonya Musa asione ajabu juu ya ukatili wa Farao, na juu ya mapigo na maafa makali ambayo ukaidi wa Farao ungeleta juu ya Wamisri (18-23). Lakini ilikuwa vigumu kwa Musa kuwafundisha Waisraeli wamtii Mungu, iwapo yeye mwenyewe hakutimiza agizo la kwanza la agano, yaani kumtahiri mwanawe (taz.Mwa 17:10,14). Mungu alimletea Musa ugonjwa au ajali ambayo nusura ingalimwua, ili kumkumbusha wajibu wa madaraka yake. Musa hakujiweza kabisa kutimiza operesheni hiyo ya kutahiri, na hivyo mkewe aliifanya kwa niaba yake. Kwa njia hii alimwokoa Musa maisha yake na kurudishiwa mume wake alipofikiri kuwa amekwisha potea (24-26).


Haruni alikuja kumlaki Musa katika Mlima Horebu, kisha wote wawili walifuatana kwenda Misri. Kama Musa alivyofikiri, Waebrania hawakumwamini hapo mwanzo, lakini walipoziona ishara zilizoongozwa na Mungu walibadili mawazo yao (27-31).


Farao afanya moyo wake kuwa mgumu

Lazima tukumbuke kwamba, kwa Mwebrania Mungu alikuwa sababu ya kwanza kwa kila jambo. Maneno ambayo sisi tungeyaona ya ajabu, mwandishi wa habari zile hakuyaona hivyo. Yeye aliona sawa kabisa aliposema kwamba Mungu alifanya moyo wa Farao uwe mgumu, au Farao alifanya moyo wake mgumu, au moyo wa Farao ukawa mgumu. Mwebrania alitumia njia mbalimbali ili aseme neno lile lile.


Kwa kweli, tusifikiri kwamba Mungu alifanya moyo wa Farao uwe mgumu wa kupinga mapenzi yake, halafu akamwadhibu kwa ajili ya kuwa na moyo mgumu. Kabla Musa hajarudi Misri, moyo wa Farao ulijaa kiburi na uasi kwa Mungu wa Israeli. Haya yalionekana wazi kwa jinsi alivyowatendea Waebrania, na yalithibitishwa tena alipomchokoza Mungu Musa alipokutana naye mara ya kwanza (5:1-2). Moyo wake ulikwisha kuwa mgumu kwa hiari yake. Alikuwa ameamua kabisa kumpinga Mungu kwa matokeo yo yote, ingawa alipewa nafasi ya kurekebisha mawazo yake zaidi ya mara moja (7:13; 8:32). Kwa njia ya kumthibitisha Farao katika ugumu wake, Mungu alionyesha ukubwa wa dhambi zake, pia alionyesha haki ya hukumu ya Mungu iliyomwadhibu (9:12; taz.Rum 9:14-18).