37:1-50:26 KUKUA KWA UKOO NA KUHAMA KWENDA MISRI

Yusufu apelekwa Misri (37:1-36)

Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu kwamba wazao wake wangekuwa watumwa katika nchi ya kigeni mpaka Wakanaani wawe tayari kwa hukumu yao. Kisha wazao wa Ibrahimu wangewaangamiza Wakanaani na kuteka nchi yao (15:13-16). Habari ndefu za Yusufu zinaonyesha jinsi Mungu alivyoongoza matukio kadiri ya makusudi yake aliyoyatabiri hapo awali.


Yusufu akiwa mwana aliyependelewa na baba yake, hakupendwa na kaka zake kumi. Wao walimchukia zaidi alipowasimulia ndoto zake zilizodokeza kwamba siku moja yeye angekuwa na mamlaka juu yao (37:1-11). Nafasi nzuri ilipotokea, kaka zake walitaka kumwua, lakini Rubeni aliokoa maisha yake (12-14). Kisha kaka zake wengine wakamwuza Yusufu kwa wafanya biashara waliokwenda Misri. Hatimaye alikuwa mtumwa katika nyumba ya Potifa, mmojawao wa maafisa wakuu wa Farao, mfalme wa Misri (25-36).


Yuda na wazao wake (38:1-30)

Hapo awali kidogo katika nchi ya Kanaani matata yalitokea katika familia ya Yakobo. Mwana wa tatu wa Yakobo alikuwa na wana watatu, na mkubwa wao alikuwa ameoa. Mwana yule alipokufa bila ya kuwa na mwana, Yuda alifanya kadiri ya desturi ya wakati ule akamwomba mwanawe wa pili, Onani, amwoe mjane Tamari (kwa muda), akitumaini kwamba kwa njia hiyo Tamari angemzaa mtoto. Kwa sheria, mtoto yule angehesabiwa kuwa mwana wa kaka yake aliyekufa, na hivyo angechukua jina la familia yake kwa urithi. Lakini Onani alikataa, kwa sababu alitaka watoto wote ambao angewazaa wawe watoto waliochukua jina lake mwenyewe. Kwa sababu ya kukataa kutimiza wajibu wa ukoo wake, Mungu alimwua (38:1-10).


Yuda alifikiri kwamba alikwisha fiwa na wana wawili kwa ajili ya Tamari, kwa hiyo alisita kumpa hata mwanawe wa mwisho, akiogopa penginepo mwana huyo naye angekufa. Hatimaye mwana huyo alipopata umri wa kutosha wa kuoa, Yuda hakutaka kumpa Tamari. Kwa hiyo Tamari alifanya maarifa ya kumlazimisha Yuda mwenyewe kuonana naye kimwili, akitumaini kwamba angeweza kumzaa mrithi. Tamari alijigeuza na kuvaa mavazi ya kahaba akafaulu kumdanganya Yuda (11-19). Baadaye, Yuda alipomwona mkwewe ana mimba, aliona nafasi nzuri ya kumwondoa moja kwa moja. Tamari akajiokoa na kumwaibisha Yuda, akidhihirisha kwamba mimba hiyo ilikuwa ya Yuda mwenyewe (20-26).


Tamari akazaa watoto mapacha, na mkubwa wao alianzisha kizazi cha Yuda mpaka kwa Daudi, na katika wazao hao mwisho alipatikana Yesu aliye Masihi (27-30; taz.Mt 1:3,6,16; Lk 3:23,31,33).


Yusufu apata mamlaka (39:1-41:57)

Tofauti na matendo na tabia ya Yuda, Yusufu aliishi bila kosa lo lote katika nchi ya Misri. Baada ya muda mfupi aliwekwa kuwa mkuu wa nyumba ya Potifa (39:1-6). Alijitahidi sana kukataa majaribu ya kushawishiwa na mke wa Potifa ili azini naye, hata mwanamke huyo akamchukia na kumfungisha gerezani (7-20). Lakini hata huko gerezani tabia yake ilikuwa haina lawama, na baada ya muda alipewa madaraka juu ya wafungwa wengine (21-23).


Miongoni mwa wafungwa wenzake, walikuwepo wawili waliokuwa maafisa wakuu wa nyumba ya Farao (40:1-4). Usiku mmoja wote wawili waliota ndoto za ajabu, na kwa sababu wale waliamini kwamba ndoto zinaweza kutabiri habari fulani, walisimulia ndoto zao kwa Yusufu. Yusufu akatabiri kwamba, baada ya siku tatu mmojawao angerudishwa katika hali na cheo chake cha zamani, na mwingine angeuawa (5-19). Utabiri huo ukaonekana kuwa kweli, lakini afisa aliyerudishiwa cheo chake hakufanya kama Yusufu alivyomwomba, yaani hakukumbusha habari za Yusufu mbele ya mfalme (20-23; taz.mst.14-15).


Baada ya miaka miwili, Farao alipowaeleza watu wake habari za ndoto iliyomhangaisha, afisa yule alimwambia habari za Yusufu mara ya kwanza (41:1-13). Matokeo yake, Yusufu aliletwa mbele ya Farao akamtafsiria ndoto zake. Akamweleza kwamba nchi ya Misri ingekuwa na miaka saba ya mavuno na chakula tele, na baadaye miaka saba yenye ukame na njaa ingefuata (14-32). Kisha Yusufu aliongeza ushauri wake ambao ungehakikisha ugawaji wa chakula cha kutosha kwa miaka yote 14 (33-36).


Farao alipendezwa na Yusufu. Licha ya kumfanya kuwa mkuu wa mpango ule wa chakula, alimpa cheo cha kutawala Misri yote (37-44). Miaka 13 ile ya kuwa mtumwa na mfungwa (taz.mst.46 na 37:2) ilikuwa imemfundisha Yusufu hekima ile ya kumtegemea Mungu katika mambo yote ambayo yaliweza kumfaa wakati huo wa utawala wa Misri. Alimwoa mwanamke wa Misri akazaa naye wana wawili (45-52). Wakati wa njaa kali ulipotokea, nchi ya Misri peke yake ilikuwa na chakula, na watu walikuja kutoka nchi nyingine ili wanunue chakula huko Misri (53-57).


Yusufu na ndugu zake (42:1-45:28)

Ndugu zake Yusufu walipofika Misri ili kununua chakula, Yusufu aliwatambua mara moja, ila wao hawakumtambua yeye (42:1-8). Badala ya kujijulisha kwao moja kwa moja, aliamua kuwajaribu, ili aone kama walibadili tabia zao baada ya miaka mingi. Yusufu hakutaka kulipiza kisasi. Hali hiyo ya ukali ilichanganyika na wema fulani iliyokusudiwa kuamsha dhamiri zao. Walitambua kwamba waliadhibiwa kwa jinsi walivyokuwa wamemtendea ndugu yao hapo awali (9-24). Matukio ya baadaye yaliwasababisha watambue wazi kwamba Mungu alishughulika nao (25-28).


Lakini ingawa wakati huo walipenda kufanya mambo yaliyokuwa haki, hawakuweza kumshawishi baba yao kuyakubali waliyomwambia (29-38).


Mwisho Yakobo hakuwa na budi kuwaruhusu wanawe kwenda Misri tena, na wakati huo walimchukua mdogo wao, Benyamini. Tabia mpya ya umoja na ya kujitolea iliwatawala wana wa Yakobo (43:1-14). Walikuwa bado wakimwogopa Yusufu (15-23), ambaye ujuzi wake wa ajabu uliwapa hisia fulani ya hofu kwamba halikuwepo jambo lo lote ambalo wangeweza kulificha mbele yake (24-34).

Jaribio kubwa zaidi liliwapata wale ndugu Yusufu alipowaweka katika hali iliyofanana na ile ya wakati walipomwuza. Aliwashtaki kwa kosa la wizi, nao ulionekana kwa Benyamini. Kisha aliwapa nafasi ya kuwa huru, kama wangemwacha Benyamini nyuma (44:1-17). Ingalikuwa rahisi kwa akina kaka hao kuondoka wakiwa huru na kumwacha Benyamini nyuma, lakini badala yake mmojawao alijitoa ili achukue adhabu kwa niaba ya Benyamini, kusudi Benyamini aweze kurudi kwa baba yake (18-34).


Mpango wa Yusufu ulisaidia. Ndugu zake waliokubali matokeo ya makosa yao ya zamani, wakati huo walikuwa wamebadilika katika tabia zao na hata katika matendo yao. Kwa hiyo, Yusufu alipojijulisha kwao haikuwepo haja ya kuwalaumu kwa makosa yao ya zamani. Badala yake aliwaonyesha kwamba alikuwa Mungu tu aliyempangia kuja Misri, ili familia ya agano iweze kuhifadhiwa wakati wa njaa kali (45:1-8). Aliwaambia kwamba njaa ingeendelea tena kwa muda wa miaka mitano, kwa hiyo waende wakawachukue Yakobo na familia zao wafike Misri ambapo yeye angeweza kuwaangalia (9-15). Farao alithibitisha mwaliko wa Yusufu akawapatia vifaa vya usafiri (16-20). Baada ya kupakia vyakula vyao katika magari ya Farao, ndugu hao walirudi nyumbani wakamwambia baba yao mambo yote yaliyotokea (21-28).


Kuhama kwenda Misri (46:1-47:12)

Walipokuwa wakihama Kanaani kwenda Misri, Yakobo na familia yake walitua katika mji wa mwisho wa Kanaani, yaani Beer-sheba ili wamwabudu Mungu. Hapo Mungu alimwambia Yakobo kwamba, ingawa yeye angekufa Misri, wazao wake siku moja wangerudi na kuitwaa Kanaani kuwa nchi yao (46:1-4). Wakati walipohama kwenda Misri, familia ya Yakobo ilikuwa na watu kama sabini hivi (5:27).


Yusufu aliyejua kwamba Wamisri hawakupenda kuishi karibu na watu waliofuga kondoo na ng'ombe, aliwaambia ndugu zake wamwambie Farao kwamba walikuwa wafugaji wa ng'ombe. Habari hii ingehakikisha kwamba Farao angewapa eneo la mbali na Wamisri ambapo wangeweza kuishi pamoja na kuongezeka bila utamaduni na dini yao kuharibiwa na Wamisri (28-34). Mpango wa Yusufu ulifanikiwa tena, na jamaa wote walipewa nafasi ya kuishi katika nchi yenye rutuba ya Gosheni ambapo Mto Nile umegawanyika kuingia baharini (47:1-12).


Mpango wa Yusufu kuwapatia watu mahitaji (47:13-26)

Yusufu asingalikuwa amepanga kwa hekima, ukame na njaa ya miaka saba vingaliangamiza nchi za Misri na Kanaani kabisa. Aliwapa watu chakula kwa malipo ya fedha zao (13-15). Halafu, walipoishiwa fedha zao, aliwapa kwa malipo ya mifugo yao (16-17), na walipoishiwa mifugo yao, walilipa kwa mashamba yao, na mwisho walijitoa wenyewe kuwa watumwa (18-19). Kwa hiyo nchi yote ilikuwa mali ya serikali, na kila mtu alifanya kazi kwa serikali, lakini kwa malipo yake Yusufu aliwapa watu chakula, mashamba na mbegu, ili waweze kupanda tena (20-24).


Inawezekana kwamba hapo mwanzo siasa ya Yusufu ilionekana kama ya kikatili, lakini baadaye watu walitambua kwamba iliwaokoa wasiangamie. Baada ya muda mfupi walipata mavuno mazuri tena, ingawa walipaswa kulipa kodi kwa serikali kama kawaida (25-26).


Maneno kwa Yusufu na wanawe (47:27-48:22)

Yakobo alipomwagiza Yusufu kwa mkazo sana kumzika Makpela, alionyesha imani yake katika ahadi za Mungu. Alijua kwamba Kanaani ingekuwa nchi ya watu wake (27-31; taz.23:17-20; 35:12; 46:4).


Wana wawili wa Yusufu, Efraimu na Manase, wakati huo walikuwa na umri wa miaka kama 20 hivi (taz.41:50; 45:6; 47:28), na Yusufu alitaka baba yake awabariki kabla ya kufa kwake. Baraka hiyo haikuwa kuwatakia heri na fanaka tu, bali iliaminiwa kuwa mbaraka kama huo ulikuwa na unabii fulani na nguvu ya kufanya maneno yake yatokee kweli. Yakobo aliwabariki Efraimu na Manase, akiwainua na kuwapa hali ya kuwa wana wa Yakobo, wasiwe wajukuu tu. Jambo hili lilimpa Yusufu haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza ambayo Rubeni aliipoteza, kwa sababu baada ya hayo, Yusufu katika wanawe wawili angerithi sehemu mbili kuliko wana wengine wa Yakobo (48:1-7; lNya 5:1-2).

Wana wote wawili wangekuwa vichwa vya makabila ya Israeli, ingawa kabila la mwana mdogo, Efraimu, lingekuwa kubwa kuliko lile la Manase (8-20). Yakobo pia alimpa Yusufu eneo lile la nchi ya Kanaani lililokuwa mali yake (21-22; taz.33:19; 34:26-29; Yn 4:5).


Utabiri kuhusu wana 12 wa Yakobo (49:1-28)

Maneno ya mwisho ya Yakobo yalitimizwa katika historia ya makabila 12 ya Israeli (49:1-2). Mwanzo Yakobo alishughulika na wana sita wa Lea (3-15); baadaye na wana wanne wa wake wadogo (16-21), na mwisho na wana wawili wa Raheli (22-27).


Rubeni angetakiwa kuwa na nguvu, lakini kwa sababu ya kukosa kujitawala alipoteza uongozi wa taifa kubwa (49:3-4; taz.35:22). Simeoni na Lawi walikuwa wakatili, na makabila yao yalitawanyika katika Israeli (5-7; taz.34:25-26). Simeoni alipoteza hali ya umoja wa kabila lake, na baadaye lilichanganyika na kabila la Yuda (Yos 19:1,9). Lakini Lawi alitawanyika kwa heshima zaidi, kwa sababu ya bidii yake ya kushindana na ibada ya miungu. Kabila lake halikuwa na urithi wa nchi, bali lilipewa miji katikati ya makabila mengine (Kut 32:26-29; Hes 35:2-8).


Kabila la Yuda lilikuwa lenye utawala, kali na lenye nguvu, kwanza katika kuwashinda maadui, pia katika kutawala makabila mengine. Kutokana na kabila hilo, ukoo wa kifalme wa Daudi ulitokea, na mfalme wake mkuu, yaani Masihi, angetawala ulimwengu wote katika wakati wa fanaka na utukufu usivyowezekana kufikiriwa (8-12; taz.Amu 1:2; 2Sam 7:16; Ufu 5:5).


Kabila la Zabuloni lililoishi pwani lilitajirika kwa njia ya biashara iliyopitishwa katika nchi yake kwenda na kutoka baharini (13; taz.Kum 33:18-19). Kabila la Isakari lilijipatia mafanikio fulani kutoka katika nchi yake yenye mashamba ya rutuba, lakini mara nyingine lilipaswa kuwatii Wakanaani wenye nguvu zaidi waliobaki na kutawala sehemu kubwa ya Vifo vya Yakobo na Yusufu (49:29-50:26)

eneo lake (14-15).


Ingawa kabila la Dani lilitolewa katika nchi yake ya asili, liliamini kwamba lilikuwa na haki ya kuishi sawa sawa na makabila mengine, lakini lilijipatia makazi mapya kwa njia ya hila na ujeuri (16-18; taz.Amu 18:1-31). Kabila la Gadi lililoishi upande wa mashariki ya Yordani, lilikuwa wazi zaidi kwa masharabulio ya maadui kuliko makabila yaliyokuwa magharibi ya Yordani, lakini askari wake walikuwa mashujaa walioweza kuwarudisha nyuma wachokozi wake (19: taz.Kum 33:20).


Kabila la Asheri lililopakana na pwani ya kaskazini liliishi katika nchi yenye rutuba ya mashamba ambayo kutokana na mizeituni yake mafuta bora ya Israeli yote yalipatikana (20; taz.Kum 33:24). Kabila lililopakana na Asheri lilikuwa la Naftali, nalo lilienea katika nyanda za juu zenye malisho ya wanyama mpaka karibu na Ziwa Galilaya (21; Kum 33:23).


Wakati wa utabiri wa Yakobo, Yusufu alikuwa katika kilele cha mamlaka yake. Inawezekana kuwa hapo awali alishambuliwa vibaya sana kwa hila, lakini Mungu alimbariki na kumpa nguvu (22-24). Makabila mawili yaliyotokana na Yusufu yalibarikiwa vile vile. Yote mawili yalikuwa makubwa kwa idadi ya watu wake, nayo kwa jumla ya eneo lake yalipewa sehemu bora kabisa katika nchi yote ya Kanaani (25-26; Yos 17:17-18). Kabila la mwisho ni la Benyamini. Lilizidi kupenda vita kwa ajili ya faida yake, nalo lilijipatia shida zaidi. Lilinusurika kufutiliwa kabisa (27-28); taz.Amu 19-21).


Vifo vya Yakobo na Yusufu (49:29-50:26)

Tena Yakobo alitia mkazo azikwe Makpela, kama ushuhuda wa mwisho kwamba alikufa katika imani ile ile ya Ibrahimu na Isaka (29:33; taz.47:29-31). Yakobo alipokufa Farao alitangaza muda rasmi wa maombolezo wa siku 70 kwa ajili yake. Farao pi a alipeleka kundi kubwa la maafisa na watumishi waende pamoja na familia ya Yakobo kwa mazishi huko Kanaani, ili watoe msaada au ulinzi wo wote kama ungetakiwa (50:1-9). Wakanaani walistaajabu kuona Wamisri walisafiri mbali sana mpaka Kanaani ili kumzika mtu ambaye bila shaka alikuwa mtu wa maana sana (10-14).


Baada ya kuishi Misri kwa miaka kumi na saba (47:28), ndugu zake Yusufu bado walikuwa na mashaka na hofu juu ya kosa walilomtendea Yusufu wakati wa ujana wake. Yusufu alisikitika kwamba walifikiri kuwa yeye angeweza kuwalipiza kisasi. Alirudia kusema kwamba yeye angewaangalia wakati wa usoni kama alivyofanya awali, kwa sababu Mungu alikuwa ametawala ubaya wao, ili yeye aweze kuwahifadhi pamoja na familia zao (15-21; 45:7).


Baada ya kufa kwa baba yake, Yusufu aliendelea kuishi muda wa miaka 50 hivi (22; taz.41:46; 45:6; 47:28). Kama vile baba yake, hata yeye aliona familia yake ikikua na kuongezeka, naye alikufa akiwa na uhakika ule ule kwamba wazao wake wangeitwaa nchi ya ahadi. Kama kwa kuonyesha imani hiyo, aliacha maagizo kwamba wakati ambao watu wa agano wangehama kwenda Kanaani, wachukue maiti yake pamoja nao (23-26; taz.Ebr 11:22). Imani yake haikutahayarishwa (Kut 13:19; Yos 24:32).