28:10-36:43 YAKOBO AIMARISHA FAMILIA

Yakobo awaoa binti wawili wa Labani (28:10-29:30)

Kabla Yakobo hajatoka Kanaani, Mungu alimtokea katika ndoto. Ingawa matendo yake yalikuwa mabaya na ya aibu, Mungu alirudia kumhakikishia ahadi za agano zilizotolewa kwa Ibrahimu na Isaka hapo awali, akimwahidi pia kwamba angemrudisha Kanaani salama (10-15; taz.l2:l-3;26:24). Yakobo akiitikia fadhili za Mungu, alitoa ahadi kwake ya kuwa mwaminifu na kumtolea sadaka kwa ukarimu. Mahali pale alipokutana na Mungu alipaita Betheli, maana yake Nyumba ya Mungu (16:22).


Kutoka Betheli Yakobo aliendelea na safari yake mpaka alipofika Harani. Mwanzoni alikutana na Raheli, binti wa mjomba yake, kisimani, naye Raheli alimpeleka nyumbani kwa baba yake Labani (29:1-14). Labani alimdanganya Yakobo, kama vile Yakobo alivyokuwa amemdanganya Isaka. Yakobo alipokuwa amefanya kazi ya Labani kwa muda wa miaka saba, kuwa malipo ya mahari kwa Raheli, Labani alimpa binti yake mwingine, Lea, badala yake. Baada ya juma moja la sherehe za ndoa ya Yakobo na Lea, Labani alimpa Yakobo Raheli pia awe mke wake wa pili, lakini kwa sharti ya kuwa Yakobo amtumikie kwa miaka mingine saba, yakiwa malipo ya pili ya mahari. Kama ilivyokuwa desturi ya nchi ile, kila mke alipewa mjakazi kama zawadi yake ya ndoa (15-30; taz.24:59).


Watoto wa Yakobo waliozaliwa Harani (29:31-30:24)

Hali ya dharau na kutompenda Lea ambayo Yakobo aliionyesha ilileta huzuni katika nyumba yake. Hamu ya Lea ya kupendwa na Yakobo inaonekana katika majina aliyowapa wanawe wanne wa kwanza (31-35). Raheli aliyeona aibu kwa sababu alikuwa hajaweza kuzaa mwenyewe, alimpa mumewe mjakazi wake, ili aweze kumzaa mwana ambaye Raheli angeweza kumpokea kuwa mwanawe. Matokeo yake yalikuwa wana wawili (30:1-8; taz.l6:l-4). Lea aliyefikiri kwamba hangeweza kuzaa tena, alifanya vivyo hivyo, na Yakobo alipata wana wawili zaidi (9-13).


Lea alipopata tunguja kidogo (ni mimea iliyotumika kwa kutengeneza dawa ambayo watu walifikiri ingewasaidia wanawake kupata mimba), Raheli alizinunua kutoka kwa Lea kwa bei ya kumpa Lea nafasi ya kuwa na Yakobo kwa usiku ule. Uchungu wa Raheli ulizidi alipogundua kwamba tunguja hazikumsaidia, lakini Lea alimpata mwana mwingine. Baada ya muda mfupi Lea alimpata mwana mwingine tena (wa sita), na baadaye alimpata mtoto wa kike (14-21). Mwishowe hata Raheli alimpata mwana, ambaye alikuwa mwana wa kumi na mmoja wa Yakobo (22-24).


Yakobo amlaghai Labani (30:25-43)

Baada ya Raheli kumzalia mwana, Yakobo aliamua kurudi Kanaani. Labani alimwambia Yakobo ataje kiwango cha mshahara wake, kwa sababu mafanikio yote ya Labani yalikuwa matokeo ya uwezo wa ufugaji wa Yakobo (25-30). Kwa mshahara wake Yakobo alidai wanyama wote wa makundi waliokuwa na mabaka, pamoja na kondoo wote waliokuwa weusi. Kwa sababu wanyama kama hao walikuwa wachache tu, Labani alikubali. Lakini baada ya hayo alijaribu kupunguza faida ya Yakobo kwa njia ya kuwaondoa kwa hila wanyama wale wenye mabaka na kondoo weusi (31-36).


Lakini Yakobo hakushindwa. Aliamua asirudi Kanaani upesi, bali atumie nafasi ya miaka iliyofuata kwa kufuga makundi ya Labani kwa kutumia akili sana. Aliwateua wanyama bora na kuwaweka pamoja, ili apate mbegu bora zaidi.


Hivyo alipata mbuzi na kondoo wengi sana waliokuwa wakubwa na wenye afya, pia waliokuwa na rangi ile iliyomfaa yeye, ambapo idadi ya mbuzi weusi na kondoo weupe (sehemu ya Labani) ilipungua, kwa upande wa wingi na kwa ubora pia. Kama vile watu wengine wa wakati ule, hata Yakobo aliamini kwamba, iwapo wanyama wakishtushwa wakati wa kupandana na kitu chenye madoadoa au mistari, hata watoto wao wangekuwa katika hali hiyo. Mafanikio yake yalitokana na uchaguzi wake bora wa wanyama, na hasa zaidi na utawala wa Mungu juu ya mambo hayo (37-43; taz.31:8-9).


Yakobo amtoroka Labani (31:1-55)

Labani na wanawe walipozidi kumchukia Yakobo, aliandaa safari ya kurudi Kanaani haraka (31:1-13). Lea na Raheli walikubaliana na uamuzi wa Yakobo, kwa sababu wao pia waliyachukia mambo ya baba yao. Alikuwa amewatumia binti zake ili ajitajirishe, lakini ilivyoonekana, hakutaka kuwashirikisha katika urithi (14-16). Kwa hiyo, walipotoroka, Raheli aliiba sanamu za miungu zilizokuwa nyumbani mwa Labani, kwa sababu kufuatana na desturi ya Mesopotamia, mtoto aliyekuwa na sanamu hizo alikuwa na haki ya urithi (17-21).


Labani alishtuka alipogundua kwamba Yakobo na familia yake walitoroka, lakini alikasirika zaidi kwa sababu walichukua sanamu zake za miungu. Alipowafuatia na kuwakuta hakuweza kuona sanamu hizo (22-35). Yakobo hakuweza kuvumilia zaidi dhuluma ya Labani, akamlaumu juu ya ugumu wa moyo wake na ukosefu wa shukrani kuhusu miaka 20 ya kazi ngumu aliyoifanya kwake (36-42).


Yakobo na Labani waliotiliana wasi wasi mkubwa sana, walifanya mapatano ya kumzuia kila mmoja asimshambulie mwenziwe. Wakasimamisha jiwe kubwa la ushuhuda wa mapatano yao, wakajikaza wenyewe kutimiza ahadi zao kwa njia ya kula chakula cha sadaka pamoja (43-55).


Maandalizi ya kukutana na Esau (32:1-32) Katika muda wa miaka 20 ya Yakobo kuishi Mesopotamia, Esau alikuwa ameimarisha nyumba yake katika nchi ya kusini karibu na Bahari ya Chumvi. Yakobo alijua kwamba, iwapo alitaka kuishi katika nchi ya Kanaani kwa usalama, ingempasa kwanza kusawazisha mambo yake na Esau. Akiwa na wasiwasi na hofu nyingi, alipeleka habari kwa Esau kwamba alikuwa anamkaribia (32:1-8).


Wakati huo Yakobo alikuwa amejifunza namna fulani ya unyenyekevu mbele ya Mungu ambao wakati alipokutana na Esau hapo awali hakuwa nao. Alimshukuru Mungu kwa baraka za wakati uliopita na kutumaini kwamba ahadi zake kwa wakati wa usoni zingempa uhakika wa kulindwa na ghadhabu ya Esau (9-12). Wakati huo huo Yakobo alifikiri kwamba ingefaa kutuma zawadi kwa mfululizo, ili zimfikie Esau, na hivyo ajipatie kibali kutoka kwake (13-21).


Yakobo alipoendelea kusafiri kusini, alivusha kwanza familia yake katika Mto Yaboki, ila yeye mwenyewe alibaki nyuma (22-24a). Usiku ule alikutana na Mungu aliyemtokea kwa mfano wa mtu aliyeshindana naye. Wakati waliposhikana na kushindana, Yakobo alitambua kwamba 'mtu' huyo alikuwa na nguvu iliyomzidi mwanadamu wa kawaida, pia alikuwa na uwezo wa kubariki. Kama ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita, Yakobo alikaza roho ili ashinde. Mwisho imani yake ya ubinafsi ilishindwa. Lakini kwa namna fulani Yakobo alishinda, kwa sababu alidai, naye alipata baraka ile ya pekee ya nguvu ya Mungu ambayo ingehakikisha ushindi kwa wakati wa usoni. Ingawa alishindwa na kunyenyekezwa, hakupotewa na ushupavu au roho yake ya kushindana. Uthabiti wake wa zamani bado alikuwa nao, lakini Yakobo wa zamani mwenye hila wakati huo alibadilishwa kuwa Israeli, maana yake shujaa wa Mungu (24-29). Kwa njia ya kumgusa kiuno na kumfanya achechemee daima, Mungu hakumruhusu Yakobo kusahau kwamba, ilikuwa kwa njia ya kushindwa tu alipata ushindi (30-32).


Kukutana na Esau (33:1-17) Inawezekana kwamba kukutana na Mungu kulikuwa jambo kubwa sana la kiroho kwa Yakobo, lakini hata hivyo siku ya pili yake ilimpasa akutane na Esau. Alifanya maarifa ya kukinga familia yake isije ikashambuliwa, kisha yeye mwenyewe alitangulia kukutana na Esau (33:1-3). Esau alionyesha roho ya upole na ya msamaha, na mkutano ambao Yakobo alikuwa ameuogopa sana ulikuwa jambo la furaha ya kuonana tena. Yakobo alikuwa amejipatia haki ya mzaliwa wa kwanza ya Esau na baraka zake kwa njia ya hila, lakini hakuweza kuzifurahia sawa sawa, mpaka alipojinyenyekeza mbele ya Esau, naye Esau alimkubali Yakobo alipopokea zawadi zake (4-11).


Esau alimwomba Yakobo amfuate kwenda Edomu, lakini Yakobo aliona afadhali asiende huko mapema. Alikuwa na familia kubwa na makundi makubwa ya mifugo, naye aliamua kwamba ingekuwa bora kama angetulia kwanza katika mji wa Sukothi uliokuwa karibu (12-17).


Katika nchi ya Kanaani tena (33:18-35:15)

Baada ya muda Yakobo alihama Sukothi akavuka Mto Yordani akaingia nchi ya Kanaani yenyewe akaishi Shekemu. Kwa njia ya kununua eneo la nchi, alipata sehemu ya nchi aliyoahidiwa na Mungu kuwa mali yake na ya wazao wake daima (18:20; taz.23:l-20; 28:1-5).


Mwana wa mkuu wa mji alipomnajisi binti wa Yakobo, Dina, mkuu wa mji ule alipendekeza kwa Yakobo kwamba mwanawe amwoe binti huyo, na wana wa Yakobo wangeweza kuwaoa wanawake wa Kikanaani (34:1-12). Wana wa Yakobo walikubali shauri hilo, ila kwa masharti ya kuwa wanaume wa Shekemu watahiriwe kwanza (13-17). Wanaume hao wakakubali, kwa sababu walifikiri wangefaidi sana kutokana na mali nyingi kama wangeoana na nyumba ya Yakobo (18-24).


Lakini wana wa Yakobo walikuwa wamewadanganya Washekemu. Baada ya kutahiriwa kwa wanaume hao, wakati wakiwa katika hali ya maumivu, hata wasiweze kujitetea, wana wa Yakobo walishambulia mji, wakawaua wanaume wote na kuteka nyara (25-29). Kwa kuzidisha kulipiza kisasi juu ya kunajisiwa dada yao, wana wa Yakobo walifungua njia kwa mashambulio mengine (30-31).


Kisha Mungu alimwambia Yakobo aende Betheli ambapo alikuwa amemtokea kabla ya miaka mingi alipokuwa akiondoka Kanaani (35:1; taz.28:l 1-22; 31:13). Lakini kabla ya hayo, wote waliokuwa pamoja na Yakobo walipaswa kuondoa miungu yo yote waliyokuwa wameileta kutoka Mesopotamia (2-4). Kwa kuona uadui juu ya nyumba ya Yakobo uliotokana na uuaji wa Shekemu, Mungu aliwapa ulinzi wa pekee wakati waliposafiri (5-8).


Huko Betheli Mungu alithibitisha ahadi zake za agano, kwa sababu wakati huo Yakobo alikuwa amerudi katika nchi aliyopewa na Mungu, naye alikuwa na familia yake pamoja naye ambayo kwa njia yake ahadi za Mungu zingetimizwa (9-15; 13:14-16; 17:2).


Habari zaidi za nyumba ya Yakobo (35:16-29)

Sehemu hii ya historia ya Israeli inamalizika kwa masimulizi ya kuzaliwa kwa mwana wa mwisho wa Yakobo (16-18), kifo cha Raheli (19-21), dhambi ya Rubeni ambayo kwa sababu yake alipoteza haki yake ya mzaliwa wa kwanza (22; taz.49:4; lNya 5:1), majina ya wana 12 wa Yakobo walioorodheshwa kwa kadiri ya utaratibu wa haki ya mama zao (23-26) na kifo cha Isaka (27-29).


Wazao wa Esau (36:1-43)

Kabla ya kueleza habari za Yakobo na familia yake zaidi, habari za Esau zinaelezwa mpaka mwisho wake. Familia ya agano (yaani ya Yakobo) iliishi Kanaani, ambapo familia isiyo ya agano (yaani ya Esau) iliishi Edomu. Huko Edomu wazao wa Esau waliongezeka sana wakawa taifa kubwa (36:1-19; taz.27:39-40). Kwa kadiri Waedomu (ndio wazao wa Esau) walivyoongezeka, wenyeji wa asili wa nchi ile, yaani Wahori, ama walilazimishwa kuhama na kuishi katika nchi nyingine, au walijiunga na kuhesabiwa kuwa Waedomu (20-30); taz.l4:6; Kum 2:12). Ripoti ile inawaorodhesha wafalme wa Waedomu wa kale (31-39) na migawanyo ya kabila la Waedomu (40-43).