10:1-1:26 ORODHA ZA VIZAZI KUTOKA NUHU MPAKA ABRAMU
Mataifa yaliyotokana na Nuhu (10:1-32)
Inavyoonekana, orodha hii iliandikwa miaka mingi baada ya wakati wa Nuhu, wazao wake walipokuwa wameongezeka sana na kuhamia katika sehemu mbalimbali. Wakati ule tofauti zao katika makabila, lugha na utamaduni zilijulikana wazi. Kusudi la kuwaorodhesha huku kulikuwa kufuatia asili za vikundi mbalimbali za watu wala siyo kuandika kila jina la wazao wa Nuhu.
Hapa pia tuna orodha iliyofupishwa na kurahisishwa, wakiteuliwa wazao sabini tu. Majina katika orodha labda hapo awali yalikuwa yale ya watu binafsi, yaliyotumiwa baadaye ili kutaja makabila yaliyotokana nao, na sehemu nyingine hata nchi fulani au miji ilipata majina kutokana na watu walioishi huko.
Wazao wengi zaidi wa Yafethi walihamia sehemu za kaskazini na kaskazini-magharibi ya Palestina, wakaenea katika nchi za Asia Ndogo na Uyunani (Ugiriki)(10:l-5). Baadhi ya wazao wa Hamu walihamia Kanaani (mpaka Waisraeli walipowanyang'anya nchi yao), pia walihamia sehemu za Mesopotamia upande wa mashariki, na sehemu za kusini wakaenea katika Misri na maeneo mengine ya magharibi ya Bahari ya Shamu (6-20). Wazao wa Shemu (Washemu) vile vile walihamia katika sehemu nyingine za Mesopotamia, pia walienea katika nchi za kusini, yaani Uarabu. Jina moja la ukoo wa Washemu, yaani Pelegi, linatajwa kwa kifupi tu katika fungu hili. Pelegi alikuwa mzazi mmojawao wa Waisraeli. Habari zake zitaonekana zaidi katika fungu lifuatalo (21-32).
Mara nyingine jina moja linatokea katika zaidi ya orodha moja, kwa sababu ya kuoana kwingi, uhamiaji, na utekaji nyara' kati ya makabila mbalimbali. Pia ikumbukwe kwamba baada ya miaka mingi katika nchi ya Kanaani, iliyoahidiwa kwa Waisraeli, waliishi watu wa makabila mbalimbali (taz. 15:18-20; 23:17-20; 34:2,30), na mara nyingine jina la kabila mojawapo liliweza kutumiwa kuwataja Wakanaani wote kwajumla (taz. 12:6; 15:16).
Maasi ya Babeli (11:1-9)
Babeli (au Babuloni) ulikuwa mji mmojawapo ulioanzishwa na Nimrodi, katika nchi ya Shinari, yaani Babeli ya kale (taz. 10:8-12). Watu wa eneo lile waliojivuna sana juu ya ustaarabu wa jamii yao, walikuwa wameendelea sana, nao walikuwa na roho ya kumpinga Mungu kama ilivyokuwa katika watu walioangamia katika gharika. Waliunganika pamoja kwa makusudi ya kujijengea mji ambao ungewapa sifa kubwa sana, pia ungewapa usalama. Waliamua kuweka kilele katika mji wao kwa kujenga jengo moja refu sana mpaka mbinguni, liwe alama ya maendeleo yao ya ustaarabu na ya uwezo wao wa kujitegemea, bila ya kuhitaji msaada wa Mungu (11:1-4).
Inawezekana kuwa jengo lao lilifanana na boma kubwa au na hekalu, lakini kwa vyo vyote, Mungu aliliona kama alama ya kumwasi Yeye. Kwa kadiri watu walivyozidi kuendelea, ndivyo walivyojaribu kutumia uwezo wao wa umoja, ili kujijengea ujamaa ambao ungewafanya huru wasiwe na haja ya msaada wa Mungu. Kwa hiyo Mungu aliangamiza umoja ule wa kuasi moja kwa moja (5-9).
Maandalio kwa Abramu (11:10-26)
Katika muda wa kati ya Nuhu na Abramu watu walikuwa wameongezeka sana katika dunia. Watu walikuwa wamehamia katika maeneo mbalimbali, katika makabila mbalimbali, na hata mataifa mazima yalikuwa yameimarika (taz. 10:1-32).
Orodha ya majina kutoka Shemu mpaka Eberi inarudia yale yaliyoandikwa katika fungu la kumi (10-15; taz. 10:21-24). Baada ya Eberi, orodha inatofautiana na ile ya fungu la kumi. Inafuata mstari wa wazao katika mwana mkubwa wa Eberi, yaani Pelegi (kwa sababu huo ulikuwa mstari alimozaliwa Abramu), ambapo orodha ya fungu la kumi ilifuata mstari wa wazao wa mwana mdogo wa Eberi, yaani Yoktani (mbari ya makabila mbalimbali ya Kiarabu (16-26; taz. 10:25-31). Orodha hii pia inaonyesha kwamba umri mrefu wa watu ulipungua, kama Mungu alivyotangaza hapo awali (taz. 6:3).
Maelezo: Inaonekana kama jina la Eberi ni chanzo moja cha jina la Ebrania. Ingawa wazao wote wa Eberi wangeweza kuitwa Waebrania, kwa kweli jina hilo likatumiwa kwa watu wa nasaba ya wazao wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo tu (14:13; 39:17; 40:15;. 43:32). Baada ya muda mrefu likawa jina lingine la Waisraeli (Kut 2:6,11; 3:18; 1 Sam 4:6; Yer 34:9; Mdo6:l;Flp3:5)